top of page

KUHUSU SISI

Kanisa la The Way limejengwa katika msingi wa Yesu Kristo, Maandiko Matakatifu kama yalivyoandikwa na kuvuviwa katika Biblia Takatifu, na uongozi wa Roho Mtakatifu. 

MAONO YETU

Kanisa linalokua kiroho na kiidadi, na lenye umoja na mshikamano.

WITO (MISSION)

Kuinua kiwango cha huduma za kanisa, na kugusa mahitaji ya jamii, hususani ya watu wanaoongea lugha ya Kiswahili.

NGUZO ZETU

Upendo, Furaha, Amani, Uvumilivu, Utu Wema, Fadhili, Uaminifu, Upole, na Kiasi.

UONGOZI

Askofu2b.jpeg

ASKOFU FERDINAND SHIDEKO

Askofu Mkuu na Mwanzilishi wa TWGC

Askofu Ferdinand Shideko ni Askofu Mkuu wa kwanza na mwanzilishi wa kanisa la The Way Gospel Church (TWGC), lenye makao yake makuu hapa Washington DC, Marekani. Alianzisha kanisa hili mwaka 2008 hapa nchini Marekani, kanisa likiitwa The Way of The Cross Gospel Ministries. Askofu Shideko ana Shahada ya pili (Master’s Degree) katika masuala ya Utangamano wa Tamaduni na Asili (Intercultural/Multicultural and Diversity Studies) kutoka Chuo Kikuu cha Trinity International University, Illnois, nchini Marekani; na ni mwanafunzi wa shahada ya udaktari wa falsafa katika masuala ya Huduma za Kanisa (PhD in Ministries) katika chuo cha Central Theological Seminary, Minnesota, nchini Marekani. Kabla ya ngazi hii ya masomo, Askofu Shideko alisoma na kuhitimu masomo ya Biblia ngazi ya Stashahada ya Juu ya Theologia (Advanced Diploma in Theology) katika Chuo cha Biblia cha Nassa (Nassa Theological College), nchini Tanzania. Askofu Shideko ni mwalimu kifani (teacher by profession). Ni mme wa mke mmoja ambaye ni Mwinjilisti na Mama Askofu Tabitha Shideko. Mungu amewabariki kwa watoto 6, wa kike 3 na wa kiume 3. Askofu Shideko alizaliwa tarehe 31/7/1958. Alimwamini Yesu mwaka 1975 na kubatizwa mwaka 1976. Alisimikwa rasmi katika ofisi ya uaskofu tarehe 20 February 2022 katika kanisa la The Way Gospel Church, Washington DC, Marekani. Ibada ya kusimikwa katika ofisi ya uaskofu iliongozwa na jopo la maaskofu likiongozwa na Askofu Rabbi Mwakanani, akisaidiana na Askofu Israel Wandaba, na Askofu John Bunango. Ilishuhudiwa na waumini wote, wachungaji, wageni waalikwa, viongozi wa ubalozi wa Tanzania nchini Marekani, na viongozi wa jumuia mbalimbali za watanzania hapa nchini Marekani. 

Merere_edited.jpg

MCH. JACOB MERERE

Mchungaji Kiongozi 

Mchungaji Jacob Leonard Merere alianza kumtumikia Mungu tangu mwaka 1996 alipojiunga na Chuo cha Vijana Wenye Wito (Youth With a Mission College) nchini Uganda. Baada ya kuhitimu masomo ya biblia nchini Uganda, Mch. Jacob alitumika kama Mwalimu wa Elimu ya Biblia katika shule mbali mbali za sekondari jijini Dar es Salaam, Tanzania. Mwaka 2000, Mungu alimpa huduma ya Uchungaji katika kanisa la International Gospel Church lenye makao yake Boston, Massachusetts, nchini Marekani. Kadhalika, mwaka 2006 alihudumu kama Mchungaji na Kiongozi wa Kusifu na Kuabudu (Praise & Worship leader) katika kanisa la Rapture Harvest Mission, Boston, Massachusetts. Mwinj. Jacob alijiunga na kanisa la The Way mwaka 2012 hadi 2013, na baadaye mwaka 2019. Kati ya mwaka 2013 hadi 2019, Mch. Jacob ametumika katika uongozi wa huduma ya East Africa Mission Fellowship iliyo chini ya kanisa la Bethel. Mwaka 2019 alisimikwa kuwa Mwinjilisti na baadaye mwaka 2020 akasimikwa kuwa Mchungaji katika kanisa la The Way Gospel Church. Kwa sasa, Mchungaji Jacob anamsaidia Mchungaji Kiongozi kama mwangalizi wa Huduma ya Umisheni, na ni mwangalizi wa kanisa la The Way Gospel Church Nevada. Mchungaji Jacob ana mke mmoja kipenzi aitwaye Irene Lusenaka Merere.

Picha - Mchungaji.jpeg

REV. JOHN KADYOLO

Mchungaji

Rev. John Kadyolo ameitwa kutumika na Bwana tangu mwaka 1985. Alisoma uchungaji katika chuo cha TAG Dodoma mwaka 1990-1992 (miaka 3). Mchungaji Kadyolo alisimikwa rasmi uchungaji mwaka 1995 katika Mkutano Mkuu wa kanisa la TAG jijini Dar es Salaam. Tangu wakati huo amesimamia makanisa yasiyopungua 5 chini ya TAG huko Tanzania. Pia amesimamia huduma ya utume katika maeneo ambayo hayajafikiwa na injili hadi mwaka 2006 kabla hajaja nchini Marekani. Akiwa nchini Marekani Mchungaji Kadyolo aliendelea kutumika katika huduma ya Unreached People hadi mwaka 2009 alipoanza kutumika kama mmoja wa wachungaji wa kanisa la The Way, mpaka mwaka 2014 aliporudi kuendeleza huduma ya Unreached People. Mwaka 2020 Mchungaji Kadyolo alirejea tena katika kanisa la The Way ambapo anamtumikia Mungu mpaka sasa, kama mwangalizi wa Huduma ya maombi na maombezi. Mchungaji Kadyolo ni mme wa mke mmoja (Mama Mch. Susan Kadyolo).

E0F0C8CA-0041-4A18-9BD5-1D1C1A9B51AD_edi

MCH. CELINA LYMO

Mchungaji

Mchungaji Celina V. Lyimo alianza utumishi mwaka 1970 alipojiunga na Chuo cha Biblia cha Mwika Bible School, Tanzania. Baadaye alipata mafunzo ya huduma ya kumfikia mtu mmoja mmoja katika huduma ya Life Ministry, jijini Dar es Salaam, Tanzania. Katika huduma hiyo hiyo, ametumika pia kama mwalimu wa watoto katika shule ya Umisheni ya Rongai mkoani Kilimanjaro; Jesus Film; pamoja na Mwalimu wa Walimu wa Uinjilisti kituo cha Nakuru Life Ministry, nchini Kenya. Baadaye, alijikita katika jamii zilizoachwa nyuma kiinjili: kama vile, jamii za Kimasai, Wasonjo, Wahazabe, Wabarbaigi, Wambugu na Wasandawe. Baada ya kuhudumu kama mwinjilisti katika kanisa la The Way kwa miaka minane, alisimikwa kuwa Mchungaji mwaka 2020. Kwa sasa Mchungaji Celina anamsaidia Mchungaji Kiongozi kuratibu Huduma ya Maombi, Familia na Ndoa, Wanawake, Ushuhudiaji na uendeshaji wa Semina mbalimbali. 

Ev_edited.jpg

MCH. MILCAH THOMAS

Mchungaji

Mchungaji Milcah Thomas ameanza huduma mwaka wa 2001 kama mwalimu wa shule ya Biblia katika chuo cha  Majahida Bible College, huko nchini Tanzania. Ev. Milcah ana Shahada ya Theologia (Bachelors degree in Theology) kutoka chuo kikuu cha Scott Christian University nchini Kenya; Shahada ya Uzamili (Masters degree) katika Ushauri wa Kichungaji (Master of Arts in Pastoral Counselling) kutoka chuo kikuu cha Liberty University, Virginia; na pia Shahada ya Maendeleo ya Kimataifa (Master of Arts in International Development) kutoka Chuo Kikuu cha Eastern University, Pennsylvania, nchini Marekani. Baada ya kutumika kama Mwinjilisti kwa muda mrefu, alisimikwa kuwa Mchungaji katika kanisa la The Way Gospel Church mnamo mwaka 2020. Kwa sasa, Mchungaji Milcah anamsaidia Mchungaji Kiongozi kama msimamizi wa huduma ya Ukarimu na Uimbaji. Mch. Milcah pia ni mwimbaji, na mmoja wa waimbaji katika kikundi cha The Sound of Glory Singers. Pamoja na huduma za kiroho, Mch. Milcah amefanya kazi ya kuhudumia wakimbizi na wahamiaji kutoka Afrika na Karibea kwa muda mrefu.

YESU NI NANI?

Maandiko matakatifu yanasema Yesu ndiye Njia, Kweli, na Uzima. Yawezekana umesikia watu wakimtaja na kumhubiri, na unapenda kumjua zaidi. Tazama hii video, na hutabaki kama ulivyo.

Video hii ni kwa hisani ya Jesus Film.

Uinjilisti
bottom of page